Wiki ya Uwekezaji Kagera sasa yaanza rasmi mkoani Kagera Agosti 12, 2019 kwa Mabalozi wa nchi tano zinazopakana na mkoa wa huo kuwasilisha fursa zinazopatikana katika nchi walizotoka na fursa hizo zinaweza kuchangamkiwa kwa namna gani na wafanyabiashara wa Kagera na Kanda ya Ziwa .

Mabalozi hao watano waliwasilisha fursa mbalimbali kwa wafanyabiashara wa mkoa wa Kagera waliohudhuria kongamano ili kuwaonesha na kuwafungua macho waweze kufanya biashara na nchi hizo. Mabalozi waliowasili mkoani Kagera ni Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Rwanda, Uganda, Kenya, Uganda na Congo DRC.

Balozi wa Tanzania Nchini Rwanda Inspekta Jenerali Mstaafu Ernest Mangu akiwasilisha fursa zinazopatikana nchini Rwanda alisema kuwa Mkoa wa Kagera unahitaji sana kuwa au kujenga masoko ya mipakani ili kusogeza bidhaa mbalimbali karibu na nchi jirani ili kuyafikia masoko kwa haraka badala ya wafanyabiashara kutoka nchi za nje kuingia ndani na kujitafutia bidhaa wenyewe..

Balozi Tanzania nchini Uganda Mhe. Dk. Aziz P. Mlima akiwasilisha fursa zinazopatikana nchini Uganda aliwashauri wananchi wa mkoa wa Kagera pamoja na wafanyabiashara kulima zao la parachichi ambalo sasa lina soko kubwa nchi za nje. “Badala ya kupanda miti ya mbao sasa ni wakati wa kulima parachichi kwa wingi.” Balozi Dk. Azizi wa Tanzania Nchini Kenya Dk. Pindi Chana pamoja na kuwasilisha fursa za biashara zinazopatikana nchini Kenya lakini alisema kuwa wafanyabiashara wa Kagera na Tanzania bado wanahitaji Elimu kubwa juu ya biashara za kimataifa kwa kuelimishwa kutumia teknolojia za mitandao badala ya kubeba bidhaa na kwenda kutafuta soko watumie teknolojia ya mitandao kupata masoko .

Balozi wa Tanzania nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Lt. Jen. (mst) Paul I. Mella alisema kuwa nchi ya Kongo ina soko kubwa la biashara na si mkoa wa Kagera tu bali Kanda ya ziwa kutokana na ukubwa nchi ya Kongo ikiwa ni pamoja na wingi wa watu wanaopatikana katika nchi hiyo.

Naye Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Burundi Dr. Edmund Kitokezi alisema kuwa Burundi kuna fursa za biashara lakini akasisitiza kuwa nchi ya Burundi isiangaliwe kwa udogo wake bali fursa za kibiashara ni kubwa kuliko mtu yeyeto anavyodhania.

Akifungua Kongamano la wafanyabiashara Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti alisistiza kuona wafanyabiashara wa Kagera na mikoa ya jirani wanaamka na kuchangamkia fursa na kuwa wasumbufu kwa viongozi wa ngazi zote katika kuhakikisha fursa za biashara zinachangamkiwa kwa kiwango kikubwa.

“Hapa tunaongelea fursa ya kitaifa na si mkoa wa Kagera tu kwani kati ya nchi nane zinazopakana na Tanzania nchi nne zote zinapakana na Mkoa wa Kagera kwa hiyo mkoa huu ni kitovu cha uchumi wa Nchi za Afrika Mashariki na Kati nataka kuona hamasa ya wafanya biashara wetu hapa wakitumia fursa hiyo.” Alisistiza MKuu wa Mkoa Gaguti.

Kwa upande mwingiene Mkuu wa Mkoa ameichagiza TCCIA kuchangamkia fursa hiyo na kufuatana naye kwenda Kutafuta masoko na Fursa zaidi za kibiashara katika nchi hizo.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Amon Mpanju alisema Mkoa wa Kagera sasa ni wakati wake wa kuinuka kiuchumi katika Awamu ya Tano na uongozi wa Mkoa usiruhusu malumbano ya kiasiasa kukwamisha maendeleo pia usiruhusu wafanyabiashara wabinafsi kuhodhi biashara wao peke yao.

Mwisho Mbunge wa Bukoba Mjini Wilfred Lwakatare aliwashukuru Mabalozi kwa kuja katika kongamano hilo na kutoa elimu hasa ya fursa zinazopatikana katika nchi walizotoka na kusema kuwa Mabalozi hao wametoa cheki ya fedha iliyowazi ili mtu kuandiaka kiasi chochote cha fedha anachohitaji akimaanisha kuwa baada ya Mabalozi kutoa elimu juu ya fursa, sasa wafanyabiashara wachague wao ni biashara gani wafanye na nchi gani.

Did you like this? Share it: